Ally Kamwe Ajibu Tetesi Za Kufungiwa Miaka Miwili Na Tff

Ally Kamwe Ajibu Tetesi Za Kufungiwa Miaka Miwili Na Tff

Kumekuwa na taarifa zinazosambaa mitandaoni zikidai kuwa Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Kamwe, amefungiwa kwa miaka miwili na Kamati ya Maadili ya TFF. Hata hivyo, Kamwe mwenyewe amekanusha madai hayo na kueleza kuwa mpaka sasa hajapokea taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka husika.

Akipiga stori katika kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM, Kamwe alisema:

“Nasema ni tetesi maana mimi, mawakili wangu wala klabu yangu hatujapewa taarifa yoyote rasmi kuhusu hukumu hiyo na mamlaka zinazohusika,” alisema Kamwe.

Akitolea ufafanuzi juu ya suala hilo, Kamwe alikiri kuitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya TFF na kufahamishwa kuwa anatuhumiwa kwa kudhalilisha mamlaka za mpira wa miguu nchini, yaani TFF na Bodi ya Ligi, kwa kutoa taarifa zisizo sahihi na zenye ukakasi kupitia ukurasa wake wa Instagram mnamo Februari 3, 2025.

Aidha, Kamwe alieleza namna ambavyo taarifa hizo zilivyomgharimu kwenye maisha yake binafsi, akifichua kuwa mama yake alipata mshtuko baada ya kusikia habari hizo.

“Mimi nimeshangaa kuona hizi taarifa, na kusema ukweli, juzi nimeshinda hospitali na mama yangu maana alipatwa na mshtuko kusikia taarifa zikienea kuwa nimefungiwa miaka miwili.”

Hadi sasa, mashabiki wa Yanga na wadau wa soka wanaendelea kufuatilia kwa karibu ili kupata ukweli wa jambo hili, huku wakisubiri tamko rasmi kutoka kwa TFF ili kuweka wazi hatma ya Ally Kamwe.