Ofisi ya Rais wa Angola imetangaza kuwa itachukua jukumu la upatanishi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na waasi wa M23 kwa lengo la kufanikisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili.
Tangazo hili limekuja baada ya Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, kufanya ziara fupi jijini Luanda na kukutana kwa faragha na mwenzake wa Angola, João Lourenço.
Hata hivyo, msemaji wa Rais Tshisekedi, Tina Salama, hakuweka wazi msimamo wa DRC kuhusu mpango huu, lakini alisema kupitia tovuti ya X kuwa Angola “itachukua hatua zinazohusiana na upatanisho.”
Hatua hii inaonekana kuwa ya muhimu katika juhudi za kurejesha amani katika eneo la Maziwa Makuu, hasa ikizingatiwa kwamba Rais Tshisekedi alikuwa ameapa kutofanya mazungumzo na waasi wa M23. Serikali ya DRC kwa muda mrefu imekataa kushiriki mazungumzo ya kikanda yanayoratibiwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hatua ambayo imekwamisha utekelezaji wa makubaliano ya Luanda, Dar es Salaam na Nairobi.
Wakati huo huo, SADC inatarajiwa kuitisha mkutano utakaohusisha Serikali ya DRC na waasi wa M23 kwa lengo la kutafuta suluhisho la amani.
Mzozo kati ya DRC na M23 umeendelea kuwa mgumu, huku DRC ikiituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao, tuhuma ambazo Rwanda imekanusha. Kwa upande wake, Rwanda imeishutumu DRC kwa kushindwa kuwaondoa wapiganaji wa kundi la FDLR, linaloendesha harakati zake ndani ya DRC dhidi ya Serikali ya Kigali.
Hatua ya Angola kuchukua jukumu la upatanishi inatarajiwa kuleta mwelekeo mpya katika juhudi za kutafuta amani, huku dunia ikisubiri kuona iwapo mazungumzo haya yatafanikiwa au yatakumbwa na changamoto kama zile za awali.
Leave a Reply