Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, ametoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuitisha mjadala wa kitaifa ili kupata maoni ya wananchi kuhusu ugawaji wa majimbo linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Amesema, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 75(4) na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2024, Ibara ya 10, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ina mamlaka ya kufanya uchunguzi na kuongeza majimbo mapya.
Mwaka 2015, zoezi kama hili lilifanyika na majimbo 26 yaliongezwa. THRDC inataka mchakato huu wa mwaka huu kuwa shirikishi, uwazi, na kuzingatia vigezo vya haki badala ya maslahi ya kisiasa.
Wakili Olengurumwa ameainisha kuwa changamoto kubwa zipo kwenye uwiano wa idadi ya watu na mgawanyo wa majimbo. Mwongozo wa ugawaji wa majimbo unataka katika vijijini jimbo liwe na angalau watu 400,000 na mijini 600,000, lakini bado kuna majimbo yanayozidi idadi hiyo lakini yanabaki kama jimbo moja, huku maeneo yenye watu wachache yakitengewa majimbo mapya.
Kwa kigezo cha kijiografia, Ngorongoro inaweza kuwa mfano halisi wa changamoto za uwakilishi, kwani ina kilomita za mraba 14,000, mara 10 ya ukubwa wa Mkoa wa Dar es Salaam. Mbunge wa eneo hilo analazimika kusafiri kilomita 200 kutoka kata moja hadi nyingine, hali inayodhoofisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kufanya uwakilishi kuwa mgumu.
THRDC inaitaka Tume ya Uchaguzi kuhakikisha kuwa ugawaji wa majimbo unazingatia vigezo vya idadi ya watu, jiografia, na ufanisi wa uwakilishi.
Aidha, amesisitiza kuwa mgawanyo huu usifanywe kwa misingi ya kisiasa, hasa katika kipindi hiki ambacho rasilimali za umma zinapaswa kudhibitiwa kwa uangalifu kutokana na kupungua kwa misaada ya wahisani kwa nchi zinazoendelea.
Wakili Onesmo Olengurumwa, amewasilisha ombi na hitaji rasmi kwa Tume huru ya Taifa Uchaguzi kuzingatia Wilaya ya Ngorongoro na maeneo mengine yote katika ugawaji wa majimbo ili kuhakikisha uwakilishi wa haki na usawa kwa wananchi wa maeneo hayo
Leave a Reply