Vijana wawili, wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 28, wamefariki dunia mkoani Arusha baada ya kupigwa na kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za wizi.
Matukio hayo yametokea katika mtaa wa Njiro Ndogo, kata ya Sokoni One, jijini Arusha. Inadaiwa kuwa chanzo cha ghasia hizo ni vitendo vya wizi wa kuvunja nyumba, uporaji wa watu njiani nyakati za usiku na alfajiri, huku wakitumia usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda, wengine wakiwaita Tatu Mzuka.
Wananchi wa eneo hilo wanasema watuhumiwa hao walikuwa wamevaa bulletproof (kinga ya risasi) ili kujilinda endapo wangepigwa risasi.
Wakati wananchi wakisimulia tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Arusha limethibitisha matukio hayo na kueleza kuwa chanzo cha vifo hivyo ni kipigo kutoka kwa wananchi waliowatuhumu kwa wizi wa pikipiki.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Justine Masejo, amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea huku akitoa onyo kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
Leave a Reply