Papa aonekana kwa mara ya kwanza tangu alazwe hospitalini

Vatican imetoa picha ya kwanza ya Papa Francis tangu alipoanza kupata matibabu katika Hospitali ya Gemelli, Rome, mwezi mmoja uliopita.

Katika picha hiyo, Papa anaonekana amekaa kwenye kiti cha magurudumu mbele ya madhabahu ndani ya kanisa la hospitali hiyo, ambako ameendelea kupata nafuu kutokana na maradhi ya nimonia.

Mapema Jumapili, Papa Francis alitoa ujumbe wa kuwashukuru wale wote waliomwombea afya njema, akisema amepitia “kipindi cha majaribio.”Aidha, alitumia fursa hiyo kuombea amani katika nchi zinazoendelea kukumbwa na vita.

Kutolewa kwa picha hiyo kumewafariji waumini wa Kanisa Katoliki na watu wengine waliokuwa na wasiwasi kuhusu afya ya kiongozi huyo wa kidini.