Washington, Marekani – Rais wa Marekani, Donald Trump, anatarajiwa kuzungumza na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, leo kuhusu juhudi za kumaliza vita vya Ukraine. Mazungumzo hayo yanakuja wakati kukiwa na ripoti za makubaliano yanayohusisha maeneo ya ardhi na udhibiti wa kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia.
Akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akipanda ndege ya Air Force One kuelekea Washington kutoka Florida, Trump alisema: “Tunataka kuona kama tunaweza kumaliza vita hivyo. Labda tunaweza, labda hatuwezi, lakini nadhani tuna nafasi nzuri sana. Nitazungumza na Rais Putin siku ya Jumanne. Kazi kubwa imefanywa mwishoni mwa juma.”
Trump anajaribu kupata uungwaji mkono wa Putin kwa pendekezo lake la kusitisha vita kwa siku 30, ambalo Ukraine ilikubali wiki iliyopita. Hata hivyo, mashambulizi makali bado yanaendelea, huku Urusi ikikaribia kuviondoa vikosi vya Ukraine kutoka eneo la Kursk, magharibi mwa Urusi.
Alipoulizwa kuhusu makubaliano yanayoweza kuzingatiwa, Trump alisema: “Tutakuwa tunazungumza kuhusu ardhi. Tutakuwa tunazungumza kuhusu mitambo ya kuzalisha umeme … Tayari tunazungumza kuhusu hilo, kugawanya baadhi ya mali.”
Ingawa hakutoa maelezo zaidi, inaaminika kuwa mazungumzo hayo yanahusisha kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, ambacho ni kikubwa zaidi barani Ulaya na kinachodhibitiwa na Urusi. Moscow na Kyiv zimekuwa zikishutumiana kwa kuhatarisha usalama wa kinu hicho.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alithibitisha kuwa Putin atazungumza na Trump kwa simu, lakini alikataa kutoa maelezo kuhusu matamshi ya Trump juu ya ardhi na mitambo ya kuzalisha umeme.
Leave a Reply