Mzozo wa DRC: M23 yajitoa mazungumzo ya amani ya Angola

FILE PHOTO: M23 rebels sit on a truck during the escort of captured FDLR members (not pictured) to Rwanda for repatriation, at the Goma-Gisenyi Grande Barrier border crossing, March 1, 2025. REUTERS/Arlette Bashizi/File Photo

Luanda, Angola – Kundi la waasi la M23, linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, limetangaza kwamba halitashiriki tena katika mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika leo mjini Luanda, Angola.

Kabla ya kujiondoa, M23 lilikuwa limethibitisha ushiriki wake katika mazungumzo hayo ya ana kwa ana na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo imesema itaendelea kushiriki mkutano huo ulioandaliwa chini ya usimamizi wa Angola.

Hatua ya M23 kususia mazungumzo imekuja baada ya Umoja wa Ulaya kutangaza vikwazo dhidi ya viongozi wa kundi hilo pamoja na makamanda wa jeshi la Rwanda. Kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X, msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, alisema: “Vikwazo vilivyowekwa kwa wanachama wetu vinaathiri kwa dhati mazungumzo ya moja kwa moja na kuzuia maendeleo yoyote.”

Licha ya hatua hiyo ya M23, msemaji wa Rais wa DRC Félix Tshisekedi amesema ujumbe wa nchi hiyo uko tayari kwa mazungumzo.

M23 ni miongoni mwa makundi yenye silaha yanayopigania udhibiti wa eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC, karibu na mpaka wa Rwanda. Mzozo huu umeendelea kuzua janga kubwa la kibinadamu, ambapo zaidi ya watu milioni saba wameyakimbia makazi yao na takriban watu 7,000 wamefariki tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, M23 inaungwa mkono na takriban wanajeshi 4,000 kutoka Rwanda, ingawa Kigali inakanusha madai hayo, ikisema vikosi vyake vinajihami dhidi ya mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wa Kongo.

Mazungumzo haya yalipangwa kufanyika kufuatia juhudi za Angola, ambayo ilitangaza mpango huo Machi 11 baada ya mazungumzo kati ya Rais Félix Tshisekedi na viongozi wa nchi hiyo.