Waziri Aweso -Sitarajii Watu Kuunganishiwa Maji Ya Bangulo Kijanja janja

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuwaunganishia maji wananchi watakaonufaika na Mradi wa Maji wa Bangulo kwa ufanisi na uaminifu na kuhakikisha hakuna mianya yoyote ya rushwa itakayojitokeza kwani kuunganishiwa maji ni haki ya msingi ya mwananchi.

Waziri Aweso ameyasema hayo leo Jumanne Machi 18, 2025 alipotembelea mradi huo uliopo mtaa wa Bangulo hali ya hewa katika kata ya Pugu Station wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam, ukitazamiwa kunufaisha wananchi 450000 wa kata mbalimbali za wilaya hiyo na wilaya jirani.

“Sitarajii na sitegemei kuona watu wanaunganishiwa maji kijanjajanja mpaka atoe hela kiasi fulani ndiyo aunganishwe, hapana. Mtu ameomba kuunganishiwa maji, DAWASA ninaomba niwaeleze, ndani ya siku saba lazima mtu aunganishiwe maji,” amesema Waziri Aweso.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amewaomba wananchi wa Bangulo kutunza vyema miundombinu ya maji katika eneo lao na kutoa taarifa watakapoona kuna dalili ya kuvuja kwa maji kutokana na baadhi ya mabomba katika eneo hilo kuwa ya muda mrefu. Amesema kwa kufanya hivyo, upotevu wa maji utadhibitiwa na huduma kwa wananchi itaendelea kutolewa kwa ufanisi.

Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama amesema mradi huo umegharimu jumla ya fedha za Kitanzania Shilingi bilioni 36.8 hii inajumuisha gharama ya ujenzi pamoja na usimamizi wa mradi ambapo kwa ujenzi pekee gharama ni Shilingi bilioni 35.0 na usimamizi wa mradi gharama ni Shilingi bilioni 1.8.

Amesema Dar es Salaam upande wa Kusini kulikuwa na changamoto ya maji kutokana na miundo ya kijiografia ya milima lakini kwa mradi huu, wananchi hawatapata shida tena kwani tayari kuna mitandao ya zamani ya maji katika eneo hilo ambayo inaendelea kuboreshwa na kutawekwa mtandao mpya.

Mradi huu unahusisha Manispaa za Ubungo, Temeke, na Jiji la Ilala, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha huduma ya maji katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji ukilenga kunufaisha wananchi 450000 wa kata wilayani Ilala za Mzinga, Kipunguni, Kitunda, Pugu station na Kiluvya huku kata za Msigani wilayani Ubungo na Kinyerezi wilayani Ilala zikienda kuongezewa msukumo wa maji.