Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Masha Mshomba amesema hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya awamu sita, katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini zimekuwa na matokeo chanya katika maeneo mbalimbali. Hivyo kwa upande wa NSSF maboresho hayo yaliyofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka minne yamekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa Mfuko, ambapo thamani ya NSSF imeongezeka kwa kutoka Shilingi trilioni 4.8 kwa mwezi Februari 2021 hadi kufikia Shilingi trilioni 9.2 kwa mwezi Februari 2025 ikiwa ni sawa ongezeko la asilimia 92.
Mafanikio mengine ni ongezeko la wanachama, ambapo kipindi cha miaka minne kilichoanzia Machi 2021 mpaka Februari 2025 NSSF imeweza kuongeza wanachama wapya wapatao 1,052,176, ambapo ongozeko hilo la wanachama limetokana na Serikali ya Awamu Sita kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha uchumi na kufungua fursa za uwekezaji na biashara na hivyo kusababisha NSSF kuongeza wanachama wapya.
Mshomba ameeleza hayo Machi 17, 2025 Jijini Dodoma wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana NSSF katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, katika kurahisisha utendaji kazi, upatikanaji wa huduma kwa wanachama na wadau popote walipo, matumizi ya TEHAMA yamekuwa ndio kipaumbele namba moja katika utendaji wa Mfuko kwani matumizi hayo yameongezeka kutoka asilimia 48 iliyokuwa imefikiwa mwezi Februari 2021, hadi kufikia asilimia 87.5 mwezi Februari 2025, huku matumizi ya TEHAMA yanatarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia 100 ifikapo Juni 2025.
Kwa upande wa uwekezaji, Mshomba ameeleza kuwa NSSF imeendelea kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika kiwanda cha sukari cha Mkulazi ambacho hadi kufikia Februari mwaka huu 2025, jumla ya tani 19,124 za sukari za majumbani zimezalishwa na kupelekwa sokoni, na kupitia kiwanda hicho fursa za ajira 8,302 zikiwa za moja kwa moja zimepatikana na ajira 6,637 zisizo za moja kwa moja.
Vile vile Mshomba alitoa wito kwa wananchi waliojiajiri katika nyanja mbalimbali za kiuchumi kujiunga na kuchangia na NSSF, kwasababu ni Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ndiyo sehemu pekee ya kuweka akiba na kupambana na majanga mbalimbali yanayosabisha umasikini wa kipato duniani kote, hivyo ni wakati sahihi wa waliojiajiri kutumia fursa iliyotolewa na Serikali ya kujiunga na NSSF.
Leave a Reply