Mkazi wa kijiji cha Kinamweli, wilaya ya Kwimba mkoa wa Mwanza, Iddy Renatus Makungu (30), amehukumiwa na mahakama ya wilaya hiyo kwenda jela miaka 60 kwa kosa la kubaka na kumsababishia ujauzito mwanafunzi (14).
Hukumu hiyo imesomwa tarehe 08.04.2025 na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Ndeko Dastan Ndeko ambapo amesema mshatakiwa huyo alitenda kosa kwa nyakati tofauti kati ya mwezi wa nne mwaka 2024 na mwezi wa tano mwaka 2024 huko katika kijiji cha Kinamweli wilaya ya Kwimba.
Kwa mujibu wa Hakimu Ndeko, mshtakiwa alitenda kosa hilo katika kesi ya jinai namba 31962 ya mwaka 2024 kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mbele ya Hakimu Ndeko, Mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Kiparo amesema kuwa Mshtakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza Mahakamani hapo tarehe 11.11.2024 na kusomewa mashtaka ya kubaka na kumpa mimba binti huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, shule ya msingi Kinamweli, ambapo mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo yote mawili.
Upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano akiwemo mhanga na Mahakama kujiridhisha kwamba upande wa mashtaka umethibitisha makosa hayo pasi na kuacha Shaka dhidi ya mtuhumiwa.
Mshtakiwa katika utetezi wake alidai kwamba amesingiziwa makosa hayo kwani awali alikuwa akifanya kazi ya kuchunga ng’ombe kwa mjomba wa mhanga huyo.
” Mheshimiwa Hakimu., nimesingiziwa kesi baada ya kudai pesa zangu za mshahara nilizochunga ng’ombe” alijitetea Makungu
Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali utetezi huo kwa kukosa mashiko na kumhukumu mshtakiwa kwenda jela miaka 30 kwa kila kosa na kuelekeza kwamba adhabu hizo zitaenda kwa pamoja na hivyo mtuhumiwa atatumikia miaka 30.
Ahukumiwa Jela Miaka 60 kwa Kubaka, Kumpa mimba Mwanafunzi

Leave a Reply