Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemtaka Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Ramadhani Kailima kuomba radhi juu ya kauli yake ya kuwa chama kisichosaini kanuni za maadili ya uchaguzi kinakosa sifa ya kushiriki uchaguzi, kwakuwa uamuzi huo haupo kwenye Katiba wala Sheria ya Uchaguzi inayotumika.
Hayo yamesema na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Rugemeleza Nshala wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Mikocheni jijini Dar es Salaam, kuhusu msimamo wa chama baada ya uamuzi wa tume hiyo, alipokuwa akijibu swali la ‘kwanini wanalalamikia uamuzi huo wa Tume, ikiwa hawana nia ya kushiriki uchaguzi’.
Aidha, Dkt. Nshala amesema kuwa licha Chadema kulalamikia uamuzi huo wa tume, bado inaendelea na msimamo wake wa kudai mabadiliko kamili, na kusisitiza kuwa kauli ya ‘No Reforms, No Election’ itaendelea kusimamiwa ipasavyo.
Mwanasheria huyo Mkuu wa Chadema, amesema kuwa Kifungu cha 162 cha sheria ya uchaguzi wa wabunge, marais na madiwani kimetoa haki kwa tume hiyo ya kuchapisha kanuni za maadili ya uchaguzi, lakini haitoi haki kwa tume hiyo kuzuia chama kushiriki uchaguzi endapo hakitasaini kanuni hizo.
Leave a Reply