Malawi yazuia kuingizwa kwa bidhaa za kilimo kutoka Tanzania

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema kuwa Serikali ya Malawi imezuia rasmi uingizwaji wa bidhaa mbalimbali za kilimo kutoka Tanzania, zikiwemo unga, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi. Bashe amesema hatua hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za wafanyabiashara wa Kitanzania wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi.

Amesema licha ya juhudi za muda mrefu za kidiplomasia, ikiwemo mawasiliano ya moja kwa moja na Waziri wa Kilimo wa Malawi, serikali haijapata majibu yoyote ya kuridhisha, hali iliyolazimu Tanzania kuandaa hatua za kulinda maslahi ya taifa.

“Kwa zaidi ya miaka mitano, tumekuwa tukijaribu kufungua soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio. Hali hii inafanana na changamoto tulizozipitia kwa zaidi ya miaka kumi kwenye suala la parachichi, hadi tulipoamua kuchukua hatua madhubuti,” amesema Mhe. Bashe.

Katika taarifa yake, Waziri Bashe ameeleza kuwa kuanzia Jumatano ijayo, endapo Malawi na Afrika Kusini hazitabadili msimamo wao, Serikali ya Tanzania itatekeleza hatua zifuatazo:

1. Kuzuia uingizwaji wa bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini.

2.Mizigo ya bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini haitaruhusiwa kupita ndani ya mipaka ya Tanzania, kuelekea bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote, hadi zuio hilo litakapoondolewa.

3. Usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi utasitishwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda maslahi ya wakulima na wafanyabiashara wa Kitanzania

Aidha, Waziri Bashe amewataka wasafirishaji wote wa Kitanzania kuacha mara moja kupakia bidhaa za kilimo zinazolengwa kuelekea nchi hizo mbili, hadi hapo watakapobadilisha misimamo yao.

“Wafanyabiashara walioweka order za apples, machungwa, na bidhaa zingine ambazo hununuliwa Afrika kusini, ninawashauri kuacha kwa sasa kwani hatutoziruhusu kuingia Tanzania mpaka hapo Afrika Kusini itakapo tufungulia soko la ndizi.”

“Ninathibitisha kuwa kama Waziri mwenye dhamana, nimewasiliana kwa njia mbalimbali na Waziri wa Kilimo wa Malawi bila mafanikio ya kupata majibu rasmi.”

“Hatua hizi ni za kulinda heshima ya nchi yetu, uchumi wa wakulima wetu, na usawa katika biashara za kikanda” – Amesema Waziri Bashe