Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameelezea masikitiko yake makubwa kufuatia kusambaa kwa video mitandaoni zikionesha wanafunzi wa kike kutoka chuo kikuu kimoja nchini wakimdhalilisha mwanafunzi mwenzao wa kike kutoka chuo kikuu kingine, Tukio ambalo limezua masikitiko miongoni mwa wananchi, huku wengi wakilaani vikali kitendo hicho.
Katika taarifa yake kwenye ukurasa wake Instagram, Dkt. Gwajima amesema kuwa ni jambo la kusikitisha sana kuona wasomi ambao wanatarajiwa kuwa mstari wa mbele katika kupigania haki na usawa, wanashiriki katika vitendo vya kikatili na vya kudhalilishana. Alisisitiza kuwa kitendo hicho ni kinyume na maadili, sheria, na utu, na kinadhalilisha wanawake wote.
Katika hatua za haraka, Waziri Gwajima amethibitisha kuwasiliana na mwanafunzi aliyeathirika (manusura) na kuhakikisha anapata huduma za ustawi wa jamii, msaada wa kisaikolojia, huduma za dawati la jinsia, na msaada wa kisheria ili haki iweze kutendeka. Aidha, ameahidi kuwasiliana na uongozi wa vyuo vikuu vinavyohusika kupitia madawati ya jinsia ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya wanafunzi waliofanya udhalilishaji huo, kwa mujibu wa sheria na miongozo ya vyuo husika.
“Pamoja na Heri ya Pasaka kwenu wote, nasikitika kuwapa taarifa kuwa, usiku wa kuamkia Jumapili ya Pasaka tarehe 20.4. 2025 nilipokea tags nyingi kupitia mtandao wa Instagram wakinitumia video kadhaa zinazoonesha mabinti kadhaa wakishirikiana kumdhalilisha binti mwingine kwa maneno na vipigo na mambo mengine mabaya ambapo, watoa taarifa walidai kuwa, mabinti hao wote ni wanafunzi wa vyuo vikuu viwili tofauti nchini huku wengine wakidaiwa kuwa, wanasoma darasa moja na huyo binti wanayemdhalilisha na kumrekodi. Aidha, kwenye mazungumzo yao kama yanavyosikika, inaonekana ni ugomvi wa kumgombania mwanaume anayetajwa kwa jina moja la Mwijaku.”
“Binafsi, nimesikitishwa sana kusikia mabinti wasomi ambao, wangetakiwa kujikita kwenye elimu na kuunganisha nguvu kupambana kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto badala yake wanatumia nguvu zao na elimu zao kukatiliana, kudhalilishana na kujidhalilisha wao kwa wao. Udhalilishaji waliofanya kwa Binti mwenzao haukubaliki kabisa na unastahili kukemewa kwa nguvu zote, kwani ni kinyume na sheria zote na pia siyo utu wala siyo haiba ya mwanamke wa Dunia ya sasa kwamba, akipishana jambo na mwanamke mwenzie au mtu yeyote, basi amfanyie udhalilishaji kwani, huko ni kujidhalilisha yeye mwenyewe na kudhalilisha wanawake wote. “
HATUA:
1. Nimewasiliana na manusura na kumuunganisha na huduma za ustawi wa jamii, msaada wa kisaikolojia na huduma za Dawati la Jinsia Polisi ambapo, pia atapata Msaada wa kisheria ili haki itendeke.
2. Nawasiliana na Wakuu wa Vyuo husika kupitia Madawati ya Jinsia kwenye Vyuo husika Ili hatua za nidhamu zichukuliwe.
3. Nawasiliana na Waziri mwenye Dhamana na Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa hatua zaidi.
WITO: tuache kumaliza migogoro kupitia utaratibu wa kudhalilisha wengine. Aidha, wanawake wenzangu wote, hima tulinde heshima na haiba yetu kwa kuungana kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto huku sisi wenyewe tukijitenga na hatua za kukatili na kudhalilisha wengine. HAKUNA ALIYE JUU YA SHERIA.” – Ameandika Waziri Gwajima
Leave a Reply