Tanzania na UAE kushirikiana Sekta ya Madini,  afya na Biashara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameungana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mhe. Abdullah Bin Zayed Al Nahyan, kushuhudia utiaji saini wa mikataba na hati za makubaliano mbalimbali kati ya Tanzania na UAE. Hafla hiyo imefanyika tarehe 05 Mei, 2025 katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Makubaliano hayo yanajumuisha nyanja muhimu za biashara, forodha, madini na afya, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.


Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa ni baina ya Shirikisho la Vyama vya Biashara na Viwanda vya UAE na Barazala la Taifa la Biashara kuhusu uanzishwaji wa Baraza la Pamoja la Biashara kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Tanzania.



Katika hatua nyingine, Serikali ya Tanzania na Serikali ya UAE zimesaini mkataba wa kushirikiana na kusaidiana katika masuala ya forodha.

Kwa upande wa sekta ya afya, makubaliano yamesainiwa kati ya Wizara ya Afya ya Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya The Emirates – Tanzania itakayojengwa mjini Bukoba, mkoani Kagera.



Pia, nchi hizo mbili zimetia saini hati ya makubaliano kuhusu ushirikiano katika uwekezaji wa sekta ya madini.