Mahakama yaelekeza Tundu Lissu aletwe mahakamani kusikiliza kesi yake Mei 19

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijiji Dar Es Salaam leo Mei 6, 2025 imeahirisha kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu hadi Mei 19, 2025, ambapo Mtuhumiwa atafikishwa Mahakama tofauti na ilivyokuwa awali, kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa kwa njia ya mtandao, huku Lissu akiwa Mahabusu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Yahya aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe nyingine, mara baada ya ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo, taarifa hiyo imeonekana kutopokelewa vyema na Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Mpale Mpoki ambapo wameieleza Mahakama hiyo kuwa hawafurahishwi kwa namna upande wa Jamhuri unavyochelewesha upelelezi wa shauri hilo, hivyo kutumia hadhara hiyo kuomba kupatiwa maelezo ya kina ni kipi hasa kinakwamisha upelelezi wa shauri hilo ambalo tangu mwanzo ilielezwa kuwa ushahidi wake uko kwenye mtandao wa YouTube.

Upande wa Jamhuri kupitia kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Yahya uliieleza Mahakama kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria kinachowalazimisha kueleza nini kimesalia kwenye upelelezi, badala yake alitumia fursa hiyo kuieleza Mahakama kuwa pindi upelelezi wa shauri hilo utakapokamilika wataweka taarifa zake kwenye mfumo ‘mtandao’ sambamba na kuwapatia Mawakili wa utetezi.

Hoja kubwa iliyowasilishwa na Mawakili wa utetezi Mahakamani leo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Godfrey Mhini ni kuhusiana na shauri hilo ni kwamba upelelezi ukamilike kwa wakati ili shauri hilo likasikilizwe Mahakama Kuu kama inavyotakiwa, kwani kuchelewesha kufanya hivyo ni kutomtendea haki mteja wao.