Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeanzisha majimbo mapya nane na kubadilisha majina ya majimbo 12 ya uchaguzi yatakayotumika kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo tarehe 12 Mei, 2025 Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema Tume imefikia uamuzi huo baada ya kupitia maombi kutoka kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Ameyataja majimbo hayo kuwa ni Jimbo la Kivule amabalo limegawanywa kutoka Jimbo la Ukonga na Jimbo la Uchaguzi la Chamanzi ambalo limegawanywa kutoka Jimbo la Mbagala yote ya mkoani Dar es Salaam.
“Mkoani Dodoma limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Dodoma Mjini limegawanywa na kuanzishwa jimbo jipya la Uchaguzi la Mtumba na Mkoani Mbeya limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Mbeya Mjini limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Uyole,” amesema.
Ameongeza kuwa Mkoani Simiyu limeanzishwa jimbo jipya moja ambapo Jimbo la Uchaguzi la Bariadi limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la uchaguzi la Bariadi Mjini.
Jaji Mwambegele amesema Mkoani Geita yameanzishwa majimbo mawili ambapo Jimbo la Uchaguzi la Busanda limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Katoro na Jimbo la Uchaguzi la Chato limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Chato Kusini.
“Mkoani Shinyanga limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Solwa limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Itwangi,” amesema.
Akizungumza kuhusu majimbo kumi na mbili (12) ya uchaguzi yaliyobadilishwa majina, Jaji Mwambegele ameyataja majimbo hayo kuwa ni pamoja na Jimbo la Uchaguzi la Chato ambalo limebadilishwa jina kuwa Jimbo la Uchaguzi la Chato Kaskazini.
“Jimbo la Uchaguzi la Nkenge limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Missenyi, Jimbo la Uchaguzi la Mpanda Vijijini limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Tanganyika na Jimbo la Uchaguzi la Buyungu limebadilishwa jina sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Kakonko,” amesema.
Leave a Reply