Bodaboda waichoma moto Daladala iliyomgonga mwenzao Arusha

Gari aina ya Hiace linalotumika kama daladala kusafirisha abiria katika eneo la Morombo, limeteketezwa kwa moto katika mtaa wa Erangau, kata ya Tetari, mkoani Arusha barabara ya East Afrika, baada ya kugonga dereva wa bodaboda aliyekuwa akivuka barabara bila kuchukua tahadhari.

Kwa mujibu wa mashuhuda, mara baada ya ajali hiyo kutokea, baadhi ya madereva wa bodaboda waliokuwa jirani na eneo la tukio walijichukulia sheria mkononi kwa kutoa mafuta kutoka kwenye pikipiki zao, kisha kusukuma gari hilo hadi mtaroni na kulichoma moto kabla ya kutokomea kusikojulikana.

“Eneo hili limekuwa hatari kwa muda mrefu. Ajali zimekuwa zikijirudia mara kwa mara na kusababisha majeraha makubwa na vifo,” alieleza mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijatoa taarifa rasmi kuhusiana na tukio hilo, ikiwa ni pamoja na hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika.

Tunaendelea kufuatilia kwa karibu ili kupata taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya tukio hili.