Wabunge wa Uganda Waidhinisha Bajeti ya Trilioni 72.4 kwa Mwaka wa Fedha 2025/26

unge la Uganda limeidhinisha bajeti ya shilingi trilioni 72.4 za Uganda (sawa na dola bilioni 20) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 unaoanza Julai, likithibitisha mabadiliko madogo kutoka matumizi ya mwaka wa fedha unaomalizika Juni, ambayo yalikuwa shilingi trilioni 72.1.

Kupitia ujumbe uliotumwa katika ukurasa rasmi wa Bunge kwenye mtandao wa kijamii X siku ya Alhamisi, bunge lilitangaza kuwa limezingatia na kupitisha mapendekezo ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikubainisha sekta zitakazonufaika zaidi na mgao wa bajeti hiyo. Hapo awali, serikali ilieleza kuwa vipaumbele vya matumizi katika mwaka huo vitajikita kwenye sekta ya kilimo, utalii na madini, hasa mafuta ya petroli.

Waziri wa Fedha, Matia Kasaija, anatarajiwa kuwasilisha bajeti hiyo rasmi bungeni tarehe 12 Juni, ambapo atatoa maelezo ya kina kuhusu matumizi yaliyopangwa na vipaumbele vya serikali.

Uganda, ambayo haina bandari, inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu kama sehemu ya maandalizi ya kuanza uzalishaji wa kibiashara wa mafuta ghafi mwaka ujao. Moja ya miradi mikubwa inayoendelea ni ujenzi wa bomba la mafuta ghafi lenye thamani ya dola bilioni 5, ambalo litatumika kusafirisha mafuta kutoka nchini humo hadi kwenye masoko ya kimataifa kupitia Tanzania.