Serikali ya Sudan Kusini imekanusha uvumi ulioenea mitandaoni ukidai kuwa Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir Mayardit, amefariki dunia.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje, serikali imeeleza kuwa habari hizo ni za uongo na zimeenezwa kwa lengo la kupotosha umma. Taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Kiir yupo hai na anaendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida.
Uvumi huo ulianza kusambaa juzi katika mitandao ya kijamii, huku baadhi ya watumiaji wakidai kuwa kiongozi huyo mkongwe wa Sudan Kusini amefariki dunia. Hata hivyo, kukanushwa kwa taarifa hizo kumekuja siku moja baada ya picha za Rais Kiir kusambaa akiwa katika shughuli rasmi, ikiwemo kushiriki mkutano wa kilele wa IGAD uliofanyika mjini Entebbe, Uganda.
Rais Kiir, ambaye ana umri wa miaka 73, kwa muda mrefu amekuwa akikabiliwa na tetesi kuhusu hali yake ya kiafya, lakini katika miezi ya hivi karibuni ameonekana mara kadhaa hadharani, akikutana na viongozi wa kimataifa pamoja na kusimamia mabadiliko ya kisera na ya kiuongozi serikalini.
Tukio hili linajiri wakati ambapo nchi hiyo inaendelea kukumbwa na mvutano wa kisiasa kati ya wafuasi wa Rais Kiir na wale wa makamu wake wa zamani, Riek Machar, ambaye kwa sasa anazuiliwa kwenye kifungo cha ndani. Hofu ya kurejea kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe imekuwa ikiongezeka, huku jumuiya ya kimataifa ikitoa wito wa maelewano ya kisiasa.
Serikali imewataka wananchi kupuuza taarifa za uzushi na kuendelea kuwa na utulivu, huku ikisisitiza kuwa Rais Kiir bado anaongoza taifa hilo.
Leave a Reply