Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Augustin Matata Ponyo, amehukumiwa kifungo cha miaka kumi cha kazi ya kulazimishwa kwa kosa la rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma.
Uamuzi huo ulitolewa na Mahakama ya Kikatiba ya Congo siku ya Jumanne, ambapo Matata Ponyo alipatikana na hatia ya kuhusika katika ubadhirifu wa kiasi cha dola milioni 245 (sawa na paundi milioni 182). Katika kesi hiyo, alihukumiwa pamoja na Deogratias Mutombo, aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya taifa hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za mahakama, sehemu ya fedha hizo zilikuwa zimekusudiwa kwa miradi mikubwa ya maendeleo ya kilimo, ambayo ilikuwa na lengo la kupunguza uhaba wa chakula nchini. Hata hivyo, fedha hizo zilidaiwa kutumiwa kinyume na taratibu, na hivyo kuleta hasara kwa taifa.
Wakili wa Matata Ponyo amesema kuwa hukumu hiyo haina msingi wa haki na kwamba imechochewa kisiasa. Akizungumza na shirika la habari la Reuters, wakili huyo alisema kuwa watachunguza njia za kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Leave a Reply