Rais Dkt. Mwinyi aipa Simba zawadi kuelekea fainali ya shirikisho Caf

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa Zawadi Maalum kwa timu ya Simba Sports Club kwa kugharamia matumizi ya Uwanja wa New Amaan Complex bila gharama yoyote kwa ajili ya kucheza fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho la CAF, itakayofanyika siku ya Jumapili, Mei 25, 2025, saa 10 jioni.

Uamuzi huo wa Rais Dkt. Mwinyi unalenga kudhihirisha mapenzi yake ya dhati kwa michezo pamoja na kuhamasisha ushindi kwa timu ya Simba SC, katika mechi hii ya kihistoria dhidi ya RS Berkane kutoka Morocco.

Hatua hiyo pia ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuunga mkono maendeleo ya michezo na kuleta hadhi ya kimataifa.

Mbali na kuruhusu matumizi ya Uwanja huo bure, Rais Dkt. Mwinyi amechukua dhamana ya kugharamia maandalizi yote muhimu ya uwanja kwa mechi hiyo.

Aidha, fainali ya mechi hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya washabiki kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa kutambua uzito wa mechi hiyo kwa Taifa, Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kuhudhuria fainali hiyo sambamba na Watanzania wote katika kuwaunga mkono Simba SC na kuhamasisha ushindi wa kihistoria.