Kesi ya Uhaini ya Lissu yaahirishwa hadi Juni 16,2025

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu hadi Juni 16, 2025 baada ya upande wa jamhuri katika kesi hiyo kueleza kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamika, na upo katika hatua za mwisho.

Uamuzi huo umetolewa leo Juni 2, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Franko Kiswaga, ambapo pia mahakama imeagiza upande wa jamhuri kuhakikisha unaharakisha na kutoa taarifa za mwenendo wa upelekezi wa kesi hiyo ili shauri lianze kusikilizwa mapema.

Katika kesi hiyo ambayo Tundu Lissu anawakilishwa na Mawakili wapato 30, awali mawakili hao walipinga kuahirisha kwa shauri hilo kwakuwa hoja zilizotolewa na upande wa Jamhuri hazikuwa na mashiko, na waliiomba mahakama kuifuta kesi hiyo ili mtuhumiwa ambaye kesi hiyo inamnyima dhamana awe huru, na endapo upelelezi utakapokamilika wanaweza kumkamata tena na kumfungulia mashtaka. Hoja ambayo mahakama iliitupilia mbali.

Kwa sasa ni muda wa mapumziko mafupi kabla ya kuendelea kusikiliza kesi ya pili ya jinai ya kutoa taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii.