Ajali yaua Watu 28 Mbeya, Rais Samia atuma salamu za Rambirambi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, kufuatia ajali mbaya ya gari iliyotokea tarehe 07 Juni, 2025, majira ya saa 01 usiku. Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mlima Iwambi, Tarafa ya Utengule Usongwe, Wilaya ya Mbalizi, kwenye barabara kuu ya Mbeya-Tunduma.

Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 830 EDP/T 148 CTD, lililokuwa limebeba shehena ya unga kutoka Dar es Salaam kuelekea Zambia. Lori hilo liligonga kwa nyuma magari mawili, Mitsubishi Rosa (T 257 DVP) na Toyota Lite Ace (T 185 DMF), kabla ya kuanguka kwenye bonde la Mto Mbalizi.

Chanzo cha ajali kinasadikiwa kuwa ni uzembe wa dereva wa lori kushindwa kulimudu gari kwenye mteremko.

Katika ajali hiyo mbaya, watu 28 wamepoteza maisha, wakiwemo wanawake 12 (kati yao watoto wawili) na wanaume 16 (kati yao watoto wawili). Hadi sasa, miili 19 imetambuliwa na tisa haijatambuliwa. Aidha, watu wanane (wanaume sita na wanawake wawili) wamejeruhiwa.

Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa madereva wote nchini kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha majanga kama hayo. Vilevile, amewapa pole wafiwa wote na anaungana na familia za marehemu na wote walioguswa na msiba huu mkubwa katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Mwenyezi Mungu awape majeruhi nafuu ya haraka na azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amin.