Miaka 10 ya wakulima kuwezeshwa, TADB yawapa mikopo ya riba nafuu ya Trilioni 1.129

Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nanenane), ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa mikopo ya riba nafuu yenye thamani ya jumla ya Shilingi Trilioni 1.129 katika kipindi cha miaka kumi kwa lengo la kuwawezesha wakulima kiuchumi.

Akizungumza leo Julai 31,2025 jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusiana na maonyesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imejikita kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta mageuzi ya kilimo kwa kumkomboa mkulima wa kawaida kupitia upatikanaji wa mikopo nafuu.

“TADB inaendelea kutekeleza wajibu wake wa msingi wa kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa wakulima, kwa masharti rafiki. Lengo letu ni kuona kilimo kinakuwa cha kibiashara na chenye tija kwa maendeleo ya taifa,” amesema Bw. Nyabundege.

Bw. Nyabundege, amesema maonyesho ya mwaka huu yatakuwa ya aina yake kwa kuwa yanaashiria mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya kilimo kupitia huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa wakulima nchini.

Maonyesho ya Nanenane mwaka huu yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 1 Agosti, huku mgeni rasmi akiwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maonyesho hayo yatawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wakiwemo wakulima, taasisi za kifedha, watafiti, na makampuni ya pembejeo kwa lengo la kubadilishana maarifa na kuonyesha mafanikio yaliyopatikana kupitia mageuzi ya sekta ya kilimo nchini.