Tume ya Nguvu za Atomu nchini Tanzania (TAEC) rasmi imesaini Hati ya Makubaliano (MoU) inayoanzisha ushirikiano na Serikali ya India kupitia Taasisi ya ‘Global Centre for Nuclear Energy Partnership’ kwa lengo la kusaidia vijana wa Tanzania kupata ufadhili wa masomo katika fani ya Teknolojia ya Nyuklia, mafunzo kwa vitendo pamoja na upatikanaji wa vifaa vya teknolojia ya nyuklia vitakavyoisaidia Tanzania kupiga hatua zaidi za kimaendeleo katika sekta ya Afya, Kilimo pamoja na Sekta nyingine Shirikishi kwa Upande wa Teknolojia ya Nyuklia.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu hapa nchini (TAEC) Prof. Najat Kassim Mohammed, amesema uwekaji saini wa Hati ya Makubaliano inayoanzisha ushirikiano huo umekuja wakati muafaka ambapo Tanzania imeanza mchakato wa kupatikana kwa umeme wa nyuklia na India tayari wamepiga hatua katika eneo hilo hivyo ushirikiano huo utaisaidia Tanzania kupiga hatua za kupatikana kwa umeme wa nyuklia.
Sambamba na hayo Prof. Najat amesema kuwa ushirikiano huo utasaidia pia kupatikana kwa semina pamoja na mafunzo ya muda mrefu ili kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu katika eneo la tafiti.
Kwa upande wake Balozi wa India hapa nchini Bishwadip Dey amesema ushirikiano wa India na Tanzania ni wa muda mrefu, Shabaha kubwa zaidi ni kuongeza nguvu, kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.
Leave a Reply