Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Mhandisi Ussi Khamis Debe, amesema shilingi bilioni 20 zitatumika kutekeleza Mradi wa Collective Actions for Disability Rights (CADiR), mradi wa miaka mitano unaolenga kuinua hali ya maisha ya watu wenye ulemavu kupitia uwekezaji katika elimu, afya, ajira na mifumo ya uwajibikaji.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa hotel ya Madinat al Bahr Mbweni – Zanzibar, Debe amesema mradi wa CADiR una malengo ya Kuboresha miundombinu ya elimu jumuishi ili kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye ulemavu, Kuimarisha huduma za afya na ukarabati unaozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.
Katibu Debe, amesema mradi huo wa miaka mitano ambao unaanza 2025 hadi mwaka 2029, unatarajia Kuongeza shule na vituo vya afya vinavyokidhi vigezo vya ujumuishaji na Kuongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu katika ajira rasmi na isiyo rasmi pamoja na Kujenga mifumo thabiti ya uwajibikaji na ushiriki wa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Watu Wenye Ulemavu wa Norway (NAD), Abdalla Amour, amesema mradi wa CADir utatekelezwa Tanzania bara na visiwani Zanzibar ukijikita katika maeneo manne makuu ambayo ni pamoja na kuzijengea uwezo wa taasisi 18 za watu wenye ulemavu,Kuongeza skuli 110 zitakazowezeshwa kutoa elimu jumuishi pamoja na Kutoa mafunzo kwa walimu, jamii na familia kuhusu ujumuishaji wa watoto wenye ulemavu.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar anatarajiwa kuuzindua rasmi mradi huo Agosti 20, mwaka huu
Leave a Reply