Mahakama yatulipia mbali maombi ya bodi ya wadhamini CHADEMA

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA, ya kuomba mahakama hiyo kutengua uamuzi wake ulioutoa Juni 10, 2025 wa kuzuia Bodi hiyo na Katibu Mkuu wa chama kutoendelea na shughuli za kisiasa kwa kutumia mali za chama.

Uamuzi huo mdogo umetolewa leo Agosti 18, 2025 na Jaji Hamidu Mwanga katika kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar Said Issa Mohammed na wenzake dhidi ya Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa Chadema kuhusu mgawanyo wa rasilimali kati ya Chama hicho Bara na Upande wa Zanazibar.

Akitoa uamuzi huo Jaji Mwanga amesema maombi ya Bodi na Katibu Mkuu wa Chadema hayana sababu za msingi za kumfanya atengue uamuzi wake, huku akizibainisha hoja kadhaa ambazo ziliwasilishwa kupitia maombi hayo, ikiwa ni pamoja na madai ya kuwa mahakama haina mamlaka ya kutoa amri ya kuzuia shughuli za kisiasa, mahakama ilisikiliza upande mmoja wakati inatoa amri hiyo na kuwa amri hiyo imesababisha mali za chama kukosa waangalizi, huku upande wa waleta maombi ukidai kuwa utaratibu ulifuatwa na upande wa wajibu maombi ulipewa fursa ya kushiriki kwenye uamuzi huo lakini hawakutaka kuitumia.

Baada ya uamuzi huo kutolewa na Jaji Mwanga, pande zote mbili zimekubaliana kuendelea na hatua inayofuata ambapo Mahakama iliahirisha shauri hilo hadi Agosti 28, 2025 kwa ajili ya mapitio ya hoja mbalimbali zinazobishaniwa na kuweka utaratibu wa kuendelea na shauri la msingi, ambalo msingi wake ni kuwa Said Issa Mohammed na wenzake wanadai kuwa Chadema imekua ikiitenga upande wa Zanzibar katika mgawanyo wa rasilimali hususani fedha.