Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limekiri kuwa linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji yaliyotokana na wivu wa mapenzi lililotokea katika Kijiji cha Ihefu, Kata ya Mdabulo, Tarafa ya Ifwagi, Wilaya ya Mufindi, mkoani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa SACP – Allan Bukumbi, amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa Agosti 20, 2025, mkulima Philimon Lalika (49) mkazi wa Ihefu, aliuawa kwa kuchomwa kisu na mke wake Elizabeth Kihombo (46), mkulima na mkazi wa kijiji hicho.
Inaelezwa kuwa tukio hilo lilitokea baada ya wawili hao kutokuelewana wakiwa nyumbani kwao, hali iliyopelekea mtuhumiwa kuchukua kisu na kumchoma mumewe tumboni, ambapo utumbo wake ulitoka nje na kusababisha kifo chake papo hapo.
Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikunywa sumu aina ya Organfosphet (dawa ya kuhifadhia nafaka) akijaribu kujiua, lakini alinusurika na kwa sasa amelazwa katika Kituo cha Afya cha Mdabulo chini ya ulinzi wa polisi.
Aidha Kamanda Bukumbi ameongeza kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi, na jeshi la polisi linaendelea na taratibu za kisheria dhidi ya mtuhumiwa huyo.
Leave a Reply