Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza kuwa liko tayari kikamilifu kuhakikisha usalama unadumishwa wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu, zinazotarajiwa kuanza rasmi kesho, Alhamisi, Agosti 28, 2025.
Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, imeelezwa kuwa Jeshi limejiandaa vya kutosha kuimarisha amani na utulivu kote nchini wakati wote wa kampeni za wagombea wa nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani, na hata baada ya kumalizika.
Taarifa hiyo pia inatoa wito maalum kwa wagombea, wafuasi wao, na wananchi kwa ujumla, kusisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kudumisha amani. Jeshi la Polisi limewataka wananchi wote kuepuka kuwa chanzo cha uvunjifu wa sheria na utaratibu ili kuepusha vurugu au uhalifu wa aina yoyote.
Pia, limesisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kuzingatia ratiba na muda uliopangwa wa kampeni ili kuepusha migogoro au migongano isiyo ya lazima. Limeonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayeshindwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa.
Leave a Reply