Uanzishwaji wa Kongani za Viwanda (Industrial Parks) ni nguzo muhimu katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira nchini. Kongani ya Viwanda inaunganisha viwanda vingi katika eneo moja, kuongeza ajira kwa vijana na kukuza Pato la Taifa (GDP) na kukuza uchumi kwa ujumla.
Hayo yamesemwa Januari 22, 2026 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), alipotembelea Kongani ya Viwanda ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukagua uanzishaji na uendelezaji wa Kongani za Viwanda ili kuongeza ajira na uzalishaji ikiwa ni utekelezaji wa Ahadi za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizozitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ndani ya siku 100.

Waziri Kapinga amebainisha kuwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Ahadi hiyo ndani ya siku 100 yameonekana kupitia utoaji wa ajira na utoaji kwa vijana ambapo hadi sasa, viwanda viwili pekee vilivyoanza kazi Kati ya viwanda 20 katika Kongani hiyo vimefanikiwa kutoa zaidi ya ajira 5,000 kwa Vijana.
Aidha, ameipongeza Kongani hiyo kwa kuanza kuongeza thamani ya bidhaa kwa kutumia malighafi za hapa nchini, ikiwemo kiwanda cha vinywaji laini kinachochakata chupa zake chenyewe.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wakurugenzi, Bi Aisha Mohammed, amebainisha kuwa kongani hiyo inayomilikiwa na kampuni za GSM, ina ukubwa wa heka 300 na inatarajiwa kuwa na jumla ya viwanda 20 ambapo hadi Sasa Viwanda viwili vinafanya kazi na
baada ya kukamilika kwa viwanda 18 vilivyobaki, jumla ya ajira 30,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zitazalishwa.
Naye Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Mabati, Bw. Mhandisi Abdullatif Said, amebainisha lengo la Kiwanda hicho ni kuzalisha bidhaa zenye viwango vya juu vya ubora kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira kwa kutumia mfumo wa kisasa unalenga kupunguza uchafuzi wa mazingira,

Akihitimisha kwa niaba ya wafanyakazi, Bw. Elia Dambani ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wake na sekta binafsi ambao umewezesha vijana wengi kupata ajira na kutoa wito kwa Serikali kuendelea kuchochea ujenzi wa viwanda zaidi nchini ili kupunguza wimbi la uhalifu mitaani kwa kutoa fursa za kiuchumi kwa vijana, jambo litakaloinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.














Leave a Reply