FCT Huchangia Kiasi Kikubwa Mazingira Bora Ya Biashara

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) amesema Baraza la Ushindani (FCT) lina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa sera ya ushindani nchini, hususan kupitia usikilizaji wa rufaa na mashauri yanayotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani pamoja na Mamlaka za Udhibiti wa Masoko.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Baraza hilo jijini Dar es Salaam Januari 26, 2026, na kusema utekelezaji huo unachangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga mazingira bora ya biashara, kuvutia uwekezaji na kulinda maslahi ya walaji na washiriki wote wa soko.

Aidha, amesema kuwa uwepo wa taasisi imara kama Baraza la Ushindani ni nguzo muhimu katika kuimarisha uchumi wa taifa, hasa katika kudhibiti vitendo vya ukiritimba na ushindani usio wa haki unaoweza kudhoofisha masoko na ukuaji wa uchumi, ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Vilevile ameongeza kuwa Baraza hilo lina haya ya kuendelea kutoa elimu kwa wadau wake na umma kwa ujumla ili kufahamika zaidi.

Kwa upande wake, Msajili wa Baraza la Ushindani, Bw. Mbegu Kaskasi, amemshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa ziara hiyo na kumhakikishia kuwa Baraza limejipanga kikamilifu kushughulikia mashauri ya rufaa kwa ufanisi na kutoa maamuzi ya haki yanayozingatia sheria na kutolewa kwa wakati, kwa lengo la kulinda maslahi ya wananchi, wafanyabiashara na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Bw. Kaskasi ameongeza kuwa Baraza linaendelea kuimarisha mifumo yake ya kazi, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali pamoja na kuendeleza utoaji wa elimu kwa wadau mbalimbali, hatua itakayoongeza ufanisi katika utoaji wa haki na kuimarisha ushindani wa soko nchini.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kufuatilia na kuimarisha utendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa lengo la kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao ipasavyo katika kulinda uchumi wa Taifa na kuchochea maendeleo endelevu ya nchi.