Tunataka Kuona DAWASA ikipunguza Upotevu Wa Maji – Kamati Ya Bunge

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imepokea na kujadili taarifa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma na kuitaka Mamlaka hiyo kuimarisha huduma Mikoa ya Dar na Pwani kwa kuhakikisha inadhibiti na kupambana na upotevu wa Maji

Mwenyekiti wa kamati ya PIC, Mheshimiwa Masanja Kadogosa amesema eneo la Kihuduma DAWASA linazidi kukua kwa makazi na uchumi na hivyo kuendelea na uhitaji wa kukamilisha miradi ya Majisafi sambamba na kubuni vyanzo vipya vitakavyosaidia uhakika wa huduma.

“Mkoa wa Dar es salaam ni kitovu cha biashara na uchumi, ni lango la biashara kwa mataifa mengi, vilevile Mkoa wa Pwani ni eneo la viwanda. Maeneo haya lazima kuwepo mikakati mahususi ya usimamizi wa huduma ili kukithi mahitaji. Simamien miradi ya kimkakati sambamba na kuhakikisha mnapambana na upotevu wa Maji” alisema Mheshimiwa Kadogosa.

Awali akiwasilisha taarifa ya DAWASA kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mkurugenzi wa Mipango, Tafiti na ufuatiliaji Ndugu Paul Sulley amesema Mamlaka inaendelea na mipango mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma ikiwemo Mradi wa Maji Bwawa la Kidunda, upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini, ununuzi wa Pampu kubwa kwa ajili ya visima virefu vya kimbiji pamoja na maandalizi ya mradi wa kutoa Maji Mto Rufiji ambayo kwa pamoja itatoa uhakika wa huduma za Maji.