Chard Talent afichua Kinachomtofautisha na Wachekeshaji Wengine

Dar es Salaam – Msanii wa vichekesho, muigizaji na mtayarishaji wa maudhui ya kidijitali ChardTalent amesema ameamua kujenga njia yake mwenyewe kwenye burudani kwa kuunganisha muziki na ucheshi kupitia mtindo anaouita Sing-a-Laugh.

ChardTalent ana zaidi ya wafuasi milioni 1.1 kwenye TikTok, 562,000+ Instagram na 428,000+ Facebook. Pia ni miongoni mwa wasanii wanaotumbuiza kwenye jukwaa la Cheka Tu. “Ninapenda watu wakitaja ChardTalent wasifikirie kichekesho tu, bali wafikirie ubunifu. Kila kazi ninayoitoa nataka iwe na kitu kipya ambacho watu hawajawahi kukiona.”

Mbali na mafanikio yake mtandaoni, ChardTalent anajulikana kwa uwezo wa kuigiza wahusika kwa kutumia lafudhi za Kimaasai, Kisukuma na Kimakonde, jambo ambalo limekuwa sehemu ya utambulisho wake. “Tanzania ina tamaduni nyingi na kila moja ina upekee wake. Mimi natumia lafudhi kama sehemu ya sanaa yangu kwa heshima, huku nikihakikisha watu wanacheka na kufurahia kazi.”

Akizungumzia malengo yake, amesema anatamani kuona muziki wa kiucheshi ukikua na kuwa sehemu muhimu ya burudani ya Tanzania na kutambulika kimataifa. “Ninaamini muziki unaweza kuchekesha, kuelimisha na kuunganisha watu kwa wakati mmoja. Ndiyo maana nitaendelea kuwekeza kwenye Sing-a-Laugh mpaka iwe alama inayotambulika ndani na nje ya Tanzania.”

Pamoja na kuendelea kutengeneza maudhui ya kidijitali, ChardTalent amesema anaandaa miradi mipya ya muziki, vichekesho na maonyesho ya jukwaani. “Kuna mambo makubwa yanakuja. Mashabiki wangu wajue bado hawajauona uwezo wangu wote. Ninaendelea kujifunza, kubadilika na kuleta burudani ya kiwango cha juu.”