Act-Wazalendo Kuja Na Mwelekeo Mpya 2025 , Yaeleza ni Mwaka Wa Kupigania Mageuzi Ya Demokrasia

Chama cha ACT-Wazalendo kupitia kwa Baraza lake la Mawaziri Kivuli leo Januari 08, 2025 limetangaza kuja na Mwelekeo mpya wakati huu ambao Taifa likijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Ubunge pamoja na Udiwani, ambao umelenga Kusimamia haki za watu wote na kuondoa hali ya Matabaka na Kuweka Usawa.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo, Isihaka Mchinjita wakati alipokuwa akitangaza Mwelekeo huo Mpya, amesema ACT kama chama cha Siasa mwaka huu wa 2025 kimedhamiria kuja na Sera zinazolenga kuijenga Tanzania kuwa Taifa la Wote na sio la Wateule Wachache.

“Tunafahamu kwamba Mwaka 2025 ni Mwaka wa Uchaguzi, kwa hiyo Sisi kama ACT-Wazalendo, Mwelekeo wetu ni kuifanya Tanzania kuwa Taifa la Wote na Kila Raia awe na Uhakika wa Kuishi, Uhakika wa matibabu, Uhakika wa Pensheni, pamoja na mambo mengine Muhimu kwa ajili ya Ustawi wake” amesema Mchinjita.

Aidha Mchinjita amesema kuwa Baraza hilo Kivuli la Mawaziri litakwenda pia kuhakikisha watanzania wanachagua mabadiliko ya kweli katika Uchaguzi mkuu unaokuja.

“Mwaka huu kwetu sisi ACT Wazalendo kupitia Baraza Kivuli la Mawaziri ni mwaka wa Kupigania mageuzi ya kidemokrasia kwa kuhakikisha tunakuwa na tume huru ya uchaguzi na mifumo bora ya sheria kwa kupinga sheria kandamizi na za kinyonyaji juu ya haki za watu” ameeleza Mchinjita.