Watu tisa wamefariki dunia na wengine 44 kujeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha basi la kampuni ya Hai Express lenye namba za usajili T 523 EKM. Basi hilo, linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es Salaam, iliyotokea leo katika eneo la Lugono, Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro, baada ya Basi hilo kugongwa na lori la mizigo.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Afisa mahusiano wa hospitali hiyo, Scholastica Nduga, amethibitisha kupokea majeruhi 44. Kati ya hao, wanawake ni 18, wanaume 19, pamoja na watoto saba.
Polisi Wanamtafuta Dereva wa Lori, Uzebembe Watajwa Kuwa Chanzo
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amethibitisha kutokea kwa ajali hii. Amesema jeshi la polisi linamtafuta dereva wa gari aina ya Scania lenye namba za usajili T.404 CZS lililokuwa limebeba shehena ya sukari, kwa tuhuma za kusababisha ajali hiyo.
Baadhi ya manusura wa ajali hiyo, akiwemo Simon Sadick, wameeleza chanzo cha ajali kuwa ni uzembe wa dereva wa lori aliyekuwa akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake, na hatimaye kugongana na basi la kampuni ya Hai Express.
Leave a Reply