Ajali za moto lindi zaua watoto kumi, Polisi yawatahadharisha wazazi

Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi limethibitisha kutokea kwa vifo kumi vya watoto wadogo vilivyotokana na ajali za moto katika kipindi cha kuanzia mwezi Februari hadi Agosti mwaka huu katika wilaya za Lindi, Kilwa, Ruangwa na Nachingwea.

Akizungumza na waandishi wa habari,kamishna msaidizi wa jeshi la polisi mkoa wa Lindi ACP John Imori amesema ajali hizo zimetokea katika maeneo tofauti mkoani hapa huku sababu zikitajwa kuwa ni wazazi au waangalizi kuelemewa na majukumu ya uzalishaji mali na kuwaacha watoto nyumbani bila uangalizi.

ACP Imori ametoa wito kwa wazazi na walezi kuchukua tahadhari kubwa ili kuepusha matukio kama hayo kutokea tena, na endapo yatajirudia jeshi halitosita kuchukua hatua za kisheria.

Katika hatua nyingine wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikianza hii leo Kamanda Imori akatumia wasaha huo kuwaasa wanachama na wakereketwa wa vyama mbalimbali vya siasa nchini kuendesha kampeni kwa njia ya amani na uitulivu ili kuepusha uvunjifu wa amani.