Al Ahly Wapokwa Alama Baada ya Kugomea Mchezo Dhidi ya Zamalek

Shirikisho la Soka nchini Misri limeipokonya klabu ya Al Ahly alama tatu na kuwapa Zamalek ushindi wa mabao matatu kwa bila, baada ya Al Ahly kugomea mchezo wa Derby dhidi ya wapinzani wao hao wa jadi.

Uamuzi wa Al Ahly kugomea mechi hiyo ulitokana na mabadiliko ya mwamuzi, ambapo mwamuzi wa Misri aliteuliwa badala ya mwamuzi wa kimataifa kama ilivyokubaliwa awali. Klabu hiyo iliwasilisha barua rasmi ya kususia mchezo huo, lakini mamlaka husika hazikubadili uamuzi, na hatimaye Al Ahly hawakutokea uwanjani.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano, Zamalek walifika uwanjani na kusubiri kwa dakika 20 bila mpinzani wao kufika, hali iliyowafanya kupewa ushindi wa mabao matatu kwa bila na pointi zote tatu.

Katika hatua nyingine, Al Ahly wametangaza kurejesha gharama zote za mashabiki wao waliokuwa wameshanunua tiketi kwa ajili ya mchezo huo.

Tukio hili limezua mjadala mkubwa katika soka la Misri, huku baadhi ya wadau wakikosoa uamuzi wa kubadilisha mwamuzi wa mchezo wa derby, jambo lililoibua sintofahamu kwa klabu na mashabiki wa mpira wa miguu.