Arsenal yabeba ubingwa wa ligi ya mabingwa Ulaya

Timu ya wanawake ya Arsenal imeandika historia kwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Women’s Champions League) kwa mara ya pili katika historia yao, baada ya kuifunga Barcelona 1-0 katika fainali iliyochezwa leo, Mei 24, 2025, kwenye Uwanja wa Estádio José Alvalade huko Lisbon, Ureno.

Arsenal ilianza vizuri katika michuano hiyo, ikishinda mechi tano za mwanzo za hatua ya makundi chini ya kocha mpya Renée Slegers.

Katika robo fainali, waliibuka na ushindi wa jumla wa 3-2 dhidi ya Real Madrid, baada ya kupindua matokeo ya 2-0 ya mechi ya kwanza kwa ushindi wa 3-0 katika mechi ya marudiano.

Nusu fainali, walikutana na Lyon na kuibuka na ushindi wa jumla wa 5-3, ikiwa ni pamoja na ushindi wa 4-1 ugenini.

Katika fainali dhidi ya Barcelona, Arsenal walionyesha nidhamu ya hali ya juu na mbinu madhubuti.

Goli pekee la mchezo lilifungwa na Stina Blackstenius dakika ya 74, baada ya pasi murua kutoka kwa Beth Mead, wote wakiwa wameingia kama wachezaji wa akiba.

Ushindi huu ni wa pili kwa Arsenal katika Ligi ya Mabingwa Wanawake, baada ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2007.

Pia, ni mara ya kwanza kwa kocha wa Kiholanzi, Renée Slegers, kushinda taji hili, na kuwa kocha wa tatu kutoka Uholanzi kushinda taji la UEFA, akifuata nyayo za Louis van Gaal na Frank Rijkaard.

Kwa ushindi huu, Arsena wameonyesha kuwa wana uwezo wa kushindana na kushinda dhidi ya timu bora barani Ulaya, na wameandika ukurasa mpya wa mafanikio katika historia ya soka la wanawake.