Baba anayetuhumiwa kumkatakata vipande mwanaye afikishwa Mahakamani

Kesi ya Mauaji ya kukusudia namba 11594/2025 inayomkabili Joseph Muhulila (28) Dereva ‘Bodaboda’ anayetuhumiwa kumuua mwanaye Timotheo Muhulila (6) kisha kumkatakata vipande na kumtumbukiza chooni imetajwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama hakimu mkazi Wilaya ya Iringa.

Imeelezwa Mahakamani hapo kuwa mnamo Aprili 11, 2025 Mshtakiwa akiwa mtaa wa Lukosi uliopo Kata ya Mkwawa Manispaa ya Iringa alimuua kwa makusudi mwanaye Timotheo Muhulila (6) kwa kukusudia kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Ikumbukwe Wasafi Media tuliripoti kwa mara ya kwanza tukio hili lililoibua hisia mseto kwa wadau wa haki za binadamu, wadau wa sheria, viongozi wa Dini na Siasa baada ya majirani walikuwa wakiishi na eneo lilipotokea tukio kuelezea hali ya tukio lilivyotokea na kufanikisha kupatikana vipande vya mwili vya nyama ya Binadamu katika shimo la choo katika nyumba aliyokuwa akiishi mshtakiwa.

Kesi hii ilikuja kutajwa kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu mkazi wa Wilaya ya Iringa Rehema Malagilo huku upande wa jamhuri ukiwakilishwa na wakili mwandamizi Radhia Njovu.

Hata hivyo Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kile kwani Mahakama hiyo haikuwa na uwezo wa kusikiliza shauri hilo hivyo Bwana Joseph Muhulila amerudishwa tena rumande hadi Mei 28, 2025 kutokana na shauri hilo kukosa dhamana kama ilivyoelekezwa katika kifungu cha 148 (5) (a) (I) sura namba 20 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya Jinai.