Bajeti Kuu ya Serikali 2025/26 ni Trilioni 56.49

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameliomba Bunge kuridhia Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26, yenye makadirio ya matumizi ya Shilingi trilioni 56.49. Bajeti hii imewasilishwa bungeni jijini Dodoma. Juni 12, 2025.

Dkt. Nchemba amefafanua kuwa bajeti hiyo inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani ya Shilingi trilioni 40.47, misaada ya Shilingi trilioni 1.07, na mikopo ya Shilingi trilioni 14.95. Akichanganua zaidi mapato ya ndani, Waziri Nchemba alibainisha kuwa mapato ya kodi yanatarajiwa kuwa Shilingi trilioni 32.31, mapato yasiyo ya kodi Shilingi trilioni 6.48, na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Shilingi trilioni 1.68. Kwa upande wa mikopo, Shilingi trilioni 6.27 zitatokana na vyanzo vya ndani, na Shilingi trilioni 8.68 zitatokana na vyanzo vya nje.

Dkt. Nchemba alieleza kuwa makadirio ya matumizi ya Serikali ya Shilingi trilioni 56.49 kwa mwaka 2025/26 yanajumuisha stahiki za watumishi na michango ya pensheni (Serikali Kuu) Shilingi trilioni 9.17, pamoja na ununuzi wa bidhaa na huduma Shilingi trilioni 5.58. Matumizi mengine muhimu ni malipo ya riba za mikopo Shilingi trilioni 6.49, ruzuku kwa taasisi za Serikali, mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa Shilingi trilioni 22.17, na Shilingi trilioni 7.72 zitatumika kugharamia malipo ya mtaji kwa deni la ndani na nje.