Baraza La Ushindani (FCT) Laimarisha Mfumo Wake Wa Usajili Wa Mashauri Kwa Njia Ya Kielektroniki

Baraza la Ushindani (FCT) limefanikiwa kuwajengea uwezo wadau na wafanyabiashara mkoani Arusha kuhusu matumizi ya mfumo wa usajili wa mashauri kwa njia ya kielektroniki (e-filing), katika mafunzo yaliyofanyika tarehe 19 Januari, 2026.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Msajili wa Baraza la Ushindani, Mhe. Mbegu Kaskasi, amesema kuwa Baraza limeunda mfumo wa kisasa wa kielektroniki unaolenga kurahisisha usajili wa mashauri na rufaa, sambamba na kupunguza gharama na usumbufu kwa wadau waliokuwa wanalazimika kufika moja kwa moja katika ofisi za Baraza hilo kwa ajili ya huduma hizo.

Ameeleza kuwa matumizi ya mfumo huo yataongeza ufanisi, uwazi na kasi katika utoaji wa haki, huku yakikwenda sambamba na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa umma.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha (RAS), Bw. Moses Pesha, amelipongeza Baraza kwa kuendelea kutoa elimu kwa wadau na wananchi, akisisitiza kuwa hatua hiyo imeongeza uelewa na imani kwa wananchi kwa kuwahakikishia kuwa wanalindwa na sheria na wanapatiwa haki zao kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo.

Naye Afisa TEHAMA wa Baraza la Ushindani, Ndg. Athumani Kanyegezi, ameeleza kuwa faida kuu ya mfumo wa e-filing ni kuimarika kwa usalama wa taarifa zinazohifadhiwa, pamoja na urahisi wa kuzifikia ndani ya muda mfupi ikilinganishwa na mfumo wa zamani wa kuhifadhi mafaili kwa njia ya kawaida.

Aidha, Bi. Jonia Karumuna, mfanyabiashara jijini Arusha, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa kuwezesha uwepo wa taasisi kama Baraza la Ushindani, ambalo limekuwa nguzo muhimu katika kulinda haki na kusikiliza rufaa zinazotokana na migogoro kutoka Tume ya Ushindani (FCC) na mamlaka mbalimbali za udhibiti ikiwemo EWURA, LATRA, TCRA, TCAA na PURA.

Amesema kuwa uwepo wa Baraza hilo umeongeza imani kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, kutokana na mchango wake katika kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati na kwa kuzingatia misingi ya ushindani wa haki nchini.