Vinara wa LaLiga, Barcelona, wameibuka na ushindi mnono wa 3-0 dhidi ya Osasuna katika mechi iliyopigwa kwenye dimba la Estadi Olímpic Lluís Companys, Barcelona.
Barca walitawala mchezo mapema, wakifunga mabao mawili kabla ya mapumziko kupitia kwa Ferran Torres na mkwaju wa penalti uliopigwa na Dani Olmo. Robert Lewandowski alihitimisha ushindi huo kwa bao la tatu dakika ya 77 ikiwa ni dakika 10 tuu baada ya kuingia ndani ya mchezo.

Kwa ushindi huu, Barcelona sasa wanaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tatu dhidi ya mabingwa watetezi, Real Madrid.
Osasuna, waliopo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, walikuwa wamewashangaza Barca kwa ushindi wa 4-2 katika mchezo wa awali msimu huu. Hata hivyo, Barcelona wamewalipiza kisasi kwa ushindi wa kishindo nyumbani, wakionyesha dhamira yao ya kutwaa taji la LaLiga.
Leave a Reply