CCM Yatoa Salamu za Rambirambi Kufuatia Kifo cha Papa Francis


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa salamu za pole na rambirambi kwa waumini wa Kanisa Katoliki na jamii ya kimataifa kufuatia kifo cha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Papa Francis, kilichotokea mapema Jumatatu.


Katika taarifa iliyotolewa na chama hicho, CCM imetoa pole za pekee kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ikiwaombea faraja, subira na nguvu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo.


CCM imemtambua Baba Mtakatifu Francis kama kiongozi wa kiroho aliyesimamia tunu za amani, mshikamano na upendo kwa wanadamu wote bila kujali tofauti za dini, rangi au mataifa. Chama hicho kimesisitiza kuwa juhudi zake za kuhubiri na kuenzi amani, haki na usawa zimeiacha dunia ikiwa salama zaidi na mahali bora pa kuishi.


“Baba Mtakatifu Francis atakumbukwa kwa juhudi zake za kuhimiza mazungumzo kati ya dini mbalimbali, utetezi wa wanyonge, na msimamo wake thabiti katika kulinda utu wa mwanadamu. Ujumbe wake wa matumaini uliwavuta watu wa imani zote na kuwahamasisha kuwa chachu ya haki, usawa, maridhiano na amani duniani,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.


Kwa niaba ya wanachama wa CCM na Watanzania kwa ujumla, chama hicho kimetoa pole kwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini na duniani kote, na kuomba Mwenyezi Mungu aipokee roho ya Baba Mtakatifu na kuilaza mahali pema peponi.