CHADEMA kwenda Mahakamani kupinga maamuzi ya Msajili

Kamati Kuu ya CHADEMA imetangaza rasmi kwenda mahakamani kupinga maamuzi na maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Uamuzi huu umefikiwa katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana Juni 3, 2025.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche amesema kuwa Kamati Kuu baada ya tafakari ya kina imeamua kwenda mahakamani kwa vile
imeshindwa kuiona nia njema ya msajli wa vyama siasa katika maamuzi yake aliyoelekeza kwenye barua aliyowapatia na taarifa yake kwa umma.

Heche amesema Kamati Kuu imewaelekeza Wanasheria wa chama hicho kuwa hadi kufika tarehe 9, Juni, 2025, shauri hilo liwe limepelekwa mahakamani na madai yao ya
msingi.

Pia, Heche amesema Sababu aliyoitoa msaįili wa vyama vya siasa ya kuzuia ruzuku ya kila mwezi kwa CHADEMA imepotoka na kwenda kinyume na sheria ya vyama vya siasa ibara 18 (6), ambayo inaeleza kuwa ruzuku itasitishwa endapo bodi ya wadhamini ya chama haina uwezo wa kusimamia fedha
za chama, kitu ambacho amedai sio sahihi,”Bodi ya wadhamini ya CHADEMA ipo chini ya Uenyekiti wa Mama Ruth Mollel na ina uwezo wa kusimamia fedha na rasilimali zote za chama”

“Msajili hana mamlaka ya kubatilisha maamuzi halali ya vikao vya chama kwa mujibu wa Katiba ya chama, Msajili wa vyama vya siasa sio mamlaka ya rufaa na sio chombo cha kupokea malalamiko yoyote kwa masuala ya chama na wanachama wa
chama cha siasa.” – amesema Heche