Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakitazingatia barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyoelekeza chama hicho kuitisha upya Baraza Kuu kwa ajili ya kuwaidhinisha viongozi walioteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, Januari 22, 2025.
Uamuzi huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, leo Jumapili Mei 25, 2025, katika kongamano la wasomi wa vyuo na vyuo vikuu Mkoa wa Dar es Salaam (CHASO), lililofanyika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni.
Heche amesema kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika Jumamosi Mei 23, 2025, kilikubaliana kwa kauli moja kutokujibu barua ya Msajili na kwamba msimamo wa chama ni kuwa maamuzi ya msajili ni batili na hayafai kufanyiwa kazi.
“Kamati Kuu imejiridhisha kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa amekwenda kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa kwa sababu hana mamlaka ya kupokea, kusikiliza na kufanyia uamuzi malalamiko ya mwanachama wa chama cha siasa,” alisema Heche.
Katika barua hiyo, Msajili alieleza kuwa akidi ya Baraza Kuu la CHADEMA haikutimia katika kikao kilichomuidhinisha Tundu Lissu kuwateua viongozi wanane, hivyo akaitaka CHADEMA kurudia mchakato huo.
Leave a Reply