CHAUMMA yapokea wanachama wapya 3,000

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Wakili Msomi Hashim Rungwe amewakaribisha wanachama wapya wapatao 3,000 waliojiunga na chama hicho rasmi leo Mei 21, 2025, na kuwataka kuwa kitu kimoja katika kutimiza lengo la kujenga chama kitakachoweza kukabiliana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa hoja.

Rungwe ametoa kauli hiyo wakati akihutubia maelfu ya wanachama waliofika katika mkutano wa maalum wa mapokezi hayo, katika ukumbi wa mikutano wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengi amesisitiza kuwa suala la ubwabwa bado litaendelea kuwa msimamo wa chama hicho kama ambavyo amekuwa akiahidi katika mikutano yake.

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Devotha Minja amesema kuwa chama hicho ni Jeshi la Ukombozi ambalo limeweka wazi kuwa litakuwa tayari kulinda haki za wanawake na watoto, kushiriki uchaguzi huru na kupigania
mabadiliko ndani ya uwanja na kushinda vita ndani ya ulingo.

“Tuingie uwanjani kwa pamoja, hatuwezi kutafuta mabadiliko tukiwa nje sio sehemu ya mchezi hatutafanikiwa, katika historia hakuna nchi yoyote iliyofanikiwa kuzuia uchaguzi, kitu pekee ambacho kinaweza kuzuia uchaguzi ni pengine ufanyike au kuwepo na vita, kinyume na hapo hauwezi kuzuia uchaguzi kwa namna yoyote,” amesema Minja.

Wanachama waliopokelewa ni kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo kutoka Kanda ya Magharibi, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Unguja na Serengeti.