COSOTA, TAA waingia makubaliano leseni za kutumia kazi za muziki kwenye viwanja vya ndege

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania COSOTA imesaini Makubaliano ya pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa ajili ya kulipia Leseni za matumizi ya kazi za Muziki katika Viwanja vyote vya Ndege nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Wasanii wananufaika na matumizi ya kazi zao.

Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile ameeleza kuwa Mamlaka inatambua umuhimu wa kulipa gharama hizo na ipo tayari kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusimamia Hakimiliki za Wasanii.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Bi. Doreen Anthony Sinare amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Bw. Abdul Mombokaleo kwa ushirikano na kuharakisha makubaliano hayo ambayo yatasaidia kuimarisha usimamizi wa hakimiliki kwa kazi za Muziki na kuongeza chachu ya ongezeko la makusanyo ya Mirabaha.

Pamoja hayo, naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Bw. Abdul Mombokaleo aliipongeza COSOTA kwa kazi kubwa inayofanya ya kusimamia hakimiliki za Wasanii katika kazi zao na Mamlaka itahakikisha 80% ya nyimbo zitakazopigwa ni za Wasanii wa Tanzania na 20% zitakuwa za nje.