Dawa mpya ya kutibu saratani ya matiti yaanza kutumika Uingereza

Dawa Mpya Yazua Tumaini kwa Waathiriwa wa Saratani ya Matiti Uingereza

Waathiriwa wa saratani ya matiti nchini Uingereza wamepata afueni kubwa baada ya kupatikana kwa dawa mpya iitwayo Capivasertib, ambayo inaonekana kuwa na ufanisi mkubwa bila madhara makubwa kama dawa nyingine za awali.

Dawa hiyo ya kisasa ina tiba mahsusi inayolenga protini ya AKT — molekuli inayochochea ukuaji wa seli za saratani. Kwa kuzuia kabisa shughuli ya protini hiyo, Capivasertib hudhibiti ukuaji wa seli hatari, hivyo kusaidia kuzuia kusambaa kwa saratani.

Kwa mujibu wa wanasayansi waliokuwa wakiifanyia kazi kwa zaidi ya miaka ishirini, Capivasertib sasa inaonekana kuwa mojawapo ya dawa zenye mafanikio makubwa zaidi kwa wagonjwa wa saratani ya hatua ya juu. Profesa Nick Turner, mtafiti mkuu na profesa wa onkolojia ya tiba katika Taasisi ya Utafiti wa Saratani na Hospitali ya Royal Marsden, alisema kuwa dawa hiyo “inatoa mbadala wenye ufanisi mkubwa, unaoweza kufanya kazi kwa muda mrefu — kwa miezi mingi, na kwa baadhi ya wagonjwa hata kwa miaka.”

Majaribio ya awali yanaonesha kuwa dawa hiyo inapunguza uvimbe kwa karibu robo ya wanawake walio na saratani ya matiti, na huendelea kufanya kazi mwilini kwa hadi mwaka mmoja.

Saratani ya matiti ndiyo aina ya saratani inayoripotiwa zaidi nchini Uingereza, ambapo mwanamke mmoja kati ya saba huathirika katika maisha yake. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 75 ya wagonjwa huendelea kuishi kwa zaidi ya miaka kumi baada ya kugunduliwa na kuanza matibabu.

Iwapo saratani itarudi na kuenea katika maeneo mengine ya mwili, lengo la matibabu huwa ni kuidhibiti, kupunguza dalili na kuboresha ubora wa maisha ya mgonjwa. Dawa ya Capivasertib inachukuliwa kama hatua mpya katika safari hiyo ya matibabu.

Dawa hii inafaa kwa wagonjwa walio na aina ya saratani ya matiti inayotegemea homoni ya oestrogen — aina ya kawaida zaidi — hasa wale wenye mabadiliko fulani ya kinasaba yanayoathiri hadi nusu ya waathirika wa aina hii ya saratani.

Kwa upande wake, Profesa Peter Johnson, Mkurugenzi wa Huduma za Saratani katika NHS England, alisema kuwa dawa hiyo ni “chaguo la ziada” kwa wagonjwa ambao saratani yao imeendelea licha ya kupokea tiba ya homoni awali, japokuwa si kila mgonjwa atakayefaa kuitumia.

Bi Claire Rowney, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la hisani la Breast Cancer Now, alisema kuwa amefarijika sana kuona dawa hiyo ikiwapa wagonjwa “tumaini la muda wa ziada wa kuishi na kutekeleza mambo yanayowapasa zaidi katika maisha yao.”

Mafanikio haya yanaendelea kuleta matumaini mapya kwa waathiriwa wa saratani ya matiti nchini Uingereza na duniani kote.