Deni la Serikali lafikia trilioni 107.70

Deni la Serikali limefikia Shilingi trilioni 107.70 hadi Aprili 2025. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Shilingi trilioni 72.94 na deni la ndani ni Shilingi trilioni 34.76.

Hayo yamebainishwa Juni 12, 2025, na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Bungeni jijini Dodoma.

“hadi Aprili 2025, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 107.70. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi trilioni 72.94 na deni la ndani ni shilingi trilioni 34.76. Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Oktoba 2024 imeonesha kuwa deni ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.”

“Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa kwa mwaka 2024/25: thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 40.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 23.6 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 123.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180.” – Amesema Dkt. Mwigulu