Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dr. Philip Isdor Mpango amesema kuwa maandalizi muhimu kwa ajili ya kufanya uchaguzi mkuu wa haki, huru na wazi yanaendelea vizuri nchini Tanzania na kutoa mwaliko kwa SADC kutuma timu ya waangalizi kwenye uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Dkt. Mpango ametoa wito huo wakati anasoma hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama jijini Antananarivo, Madagascar
Dkt. Mpango ambaye anamwakilisha Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo ametaja mafanikio kadhaa ya uenyekiti wa Tanzania katika Asasi hiyo, iliyopewa jukumu la kusimamia masuala ya ulinzi, amani na usalama katika kanda ya SADC.
Akibainisha mafanikio hayo, Dr. Mpango alieleza kuwa mwaka mmoja wa Rais Samia katika Asasi hiyo, eneo la SADC limesalia kuwa tulivu, isipokuwa mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo jitihada za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo zinaendelea.
Jitihada hizo ni pamoja na majadiliano kupitia Mpango wa Luanda na Nairobi na hatua zilizochukuliwa na Wakuu wa Nchi katika mikutano ya pamoja ya EAC na SADC. Alisema kupitia mikutano hiyo jopo la Wazee wa Hekima kusuluhisha mgogoro huo limeundwa, timu za wataalamu kutoka EAC, SADC na AU zimeunganishwa ili zifanye kazi kwa pamoja, utaratibu (roadmap) na hadidu za rejea za namna ya kusghulikia mgogoro huo zimetayarishwa.
Dkt. Mpango alisisitiza umuhimu wa migogoro inayoibuka Afrika kutafutiwa suluhu na Waafrika wenyewe, kwa nchi hizo kuwa na dhamira ya dhati na kujitoa kwa hali na mali.
Aliendelea kwa kueleza kuwa katika kipindi cha uenyekiti, Tanzania pia imeongoza programu mbalimbali zinahusu uzuiaji na usuluhishi wa migogoro, upelekaji wa vikosi vya kulinda amani kwenye maeneo ya machafuko ya kisisasa, uimarishwaji wa taasisi imara za kidemokrasia ikiwa ni pamoja na kuongoza timu za waangalizi wa uchaguzi katika nchi za Botswana, Namibia, Mauritius na Msumbiji.
Amehitimisha kwa kueleza kuwa Tanzania imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kuwa kanda ya SADC inasalia kuwa tulivu na salama na kuahid kuwa nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika kwa mwenyekiti mpya wa asasi hiyo ambayo ni Malawi.
Leave a Reply